Katika ziara yangu ya mashinani leo, vile vile nimeweza kufika katika shule ya upili ya Madunguni, Wadi ya Kakuyuni, ambayo imeathirika pakubwa na mafuriko yanayoendelea kushuhudiwa Kilifi.
Zaidi ya familia elfu moja zimeathirika na janga la mafuriko eneo hilo, na baadaye nilitangamana na wakazi katika zoezi la ugawaji chakula, angalau kiwakimu katika kipindi hiki kigumu. Hali itakaporudi sawa, nitahakikisha wakazi eneo hilo wanapata mbegu na mbolea ili wazalishe chakula cha kutosha mashambani.
Aidha, kuanzia juma lijalo, tutaikarabati zahanati ya Madunguni ambayo paa lake limekuwa likivuja kwa muda sasa. Tayari nimetuma maafisa wangu kuhakikisha shughuli hiyo inatekelezwa mara moja ili huduma za matibabu zisiathirike na mvua ya masika inayoendelea kunyesha sehemu tofauti hapa Kilifi.