Leo Kilifi Kaskazini imesema tufungue barabara za mashinani, tuboreshe huduma za afya kwa kuajiri wauguzi zaidi, maji yapatikane kila wakati na zaidi, ajira kwa vijana. Kwa sasa, tayari tumeanza kuajiri vijana, akina mama na watu wanaoishi na uatilifu takriban 2,000 kaunti nzima, ambao watasafisha mabomba ya maji, kuzoa taka na kusafisha miji yetu, kazi hizi hazihitaji kiwango chochote cha elimu.
Fauka ya hayo, natumia fursa hii kutangaza kufungwa kwa shule zote za Chekechea kaunti ya Kilifi kuanzia kesho hadi juma lijalo. Hii ni kutokana na kimbunga kikali kinachoendelea kushuhudiwa maeneo tofauti Kilifi ambapo imepelekea kupoteza maisha ya mwanafunzi mmoja kule Mariakani, wengine kujeruhiwa na kusababisha hasara kubwa ya mali maeneo tofauti.
Wakazi wangu wa Kilifi naomba tuwe waangalifu katika kipindi hiki, zaidi nawahakikishia kwamba, pamoja na baraza langu la mawaziri, tutatekeleza yote ya muhimu ambayo mnazidi kutuagiza kama viongozi wenu.