Inanipa furaha kuona Mataifa mbalimbali ulimwenguni yana uchu wakufahamu lugha ya Kiswahili kwa ufasaha. Mapema leo, nimejumuika na wanafunzi kutoka kwa zaidi ya vyuo vikuu sita vya mataifa ya kigeni, wakiongozwa na chuo kikuu cha Howard, ambao wamekuja Kilifi kwa mafunzo ya lugha ya Kiswahili katika chuo kikuu cha Pwani.
Ningependa kuwapongeza wahadhiri wanaofanikisha swala hili, wakiongozwa na Naibu Mhadhiri Mkuu katika chuo kikuu cha Pwani, Profesa Paul Mwashimba Guyo kwa kuchukua jukumu la kuhakikisha lugha hii inazungumzwa kila kona ya ulimwenguni. Kiswahili inafaa iwe lugha inayotumiwa katika shughuli rasmi kote barani Afrika, hatua ambayo naamini italeta taswira ya utangamano kwa Wananchi wa bara hili.
Kama kaunti, tunaendelea kushirikiana na vyuo hivi pamoja na wafadhili na tayari tuko na vijana wanne ambao walipata ufadhili wa masomo katika mataifa ya kigeni, lengo ni kukuza sekta ya elimu hapa Kilifi. Tunasema Kiswahili kitukuzwe ndani na nje ya Nchi!