Nimefanya kikao na baadhi ya wanachama wa kikundi cha Watamu Elimisha (CBO) kutoka Wadi ya Watamu kujadili maswala mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo uanzishwaji wa manispaa mpya ya Watamu, kwa lengo la kuikuza na kuiendeleza kaunti yetu.
Chini ya uongozi wa Mwenyekiti wao, Elisha Washe, wanachama hao wametoa maoni yao kuhusu fursa za ajira kwa vijana wa Watamu na maendeleo ya kurejesha uhai katika mji huo, haswa katika sekta za utalii, biashara, na utoaji wa huduma za umma za kaunti kupitia manispaa hiyo.
Nimewahakikishia ushirikiano wangu katika kutimiza baadhi ya matakwa yao, na nitaendelea kumjumuisha mwananchi katika utawala na uongozi wangu ili kuleta mikakati inayolenga kutatua changamoto zinazotukumba na kuboresha mazingira kwa wananchi kujiendeleza na kuwa mstari wa mbele kuchangia kufikia malengo ya ugatuzi.